MAMA RWAKATARE AFIKISHWA POLISI

By
Advertisement

MAMA RWAKATARE AFIKISHWA POLISI

Waandishi Wetu
MCHUNGAJI Kiongozi wa Kanisa la Mikocheni B Assemblies of God jijini Dar, Dk. Getrude Rwakatare (pichani) amefunguliwa mashitaka katika Kituo cha Polisi Wazo Hill kwa uharibifu wa mali inayodaiwa ina thamani ya shilingi milioni 20.
Bw. Grayson Justine anayelalamika kuvunjiwa nyumba yake na Mch. Getrude Rwakatare.
Taarifa zilizopatikana katika kituo hicho zenye Jalada la Kumbukumbu WH/RB/9029/2014 UHARIBIFU WA MALI na kuthibitishwa na mlalamikaji aliyejitambulisha kwa jina la Grayson Justine, zinaeleza mchungaji huyo alivunja nyumba ya Grayson kwa greda hali iliyomfanya mmiliki huyo kuzimia na kulazwa Zahanati ya Mico iliyopo Wazo Hill baada ya presha kupanda.
Katika mahojiano na waandishi wetu katika Ofisi za Global Publishers, Bamaga- Mwenge, Dar wiki iliyopita, Grayson alikuwa na haya ya kusema:
“Kiwanja nilichojengea nyumba nilikinunua kwa Jumanne Rajab, Agosti 24, 2011 na makubaliano yalifanyika kwa kuandikishiana Ofisi za Serikali ya Mtaa wa Bunju ‘B’ na kila mmoja alikuwa na mashahidi wake.
Nyumba ya Bw. Grayson Justine iliyobomolewa kwa greda.
“Kutokana na kuchoka katika kupangisha, niliamua kuchukua mkopo wa shilingi milioni 20 kazini ili nijenge haraka na kuhamia, ujenzi ulianza Septemba 21,  mwaka 2013 mpaka kufikia mwezi huu (Novemba) nilibakiza kupaua na nilitarajia kuhamia mwanzoni mwa mwaka kesho.
“Baadaye nilikwenda Moshi kwenye msiba wa baba, niliporudi Dar nilimaliza siku moja tu, nikaripoti kazini. Nikiwa kazini Novemba 11, mwaka huu nikapigiwa simu na jirani kwamba nyumba yangu inabomolewa na greda, alifikiri kwamba nimeshaonana na Mchungaji Rwakatare na kukubaliana naye.
“Nilikwenda kule, kufika nikakuta hakuna jengo! Nilidondoka chini, sikujua kilichoendelea, nilipoteza fahamu, nilijitambua nikiwa Zahanati ya Mico.
“Kinachoniumiza sana ni kitendo cha kuvunjiwa nyumba yangu bila kushirikishwa, bora hata angenifungulia mashitaka kama anaona nilivamia kikwanja chake.”
“Yeye ana uwezo, ana ghorofa ya zaidi ya shilingi bilioni moja iweje anionee na kunivunjia mimi maskini niliyejenga kwa fedha za mkopo?
Mch. Getrude Rwakatare.
“Kituo cha polisi nilifika karibu mara nne lakini mpaka leo hii sijapewa mpelelezi wala hawajafika eneo la tukio, nataka sheria ichukue mkondo wake.”
Mwandishi alifika katika eneo la tukio na kushuhudia kifusi kinachodaiwa kuwa ni iliyokuwa nyumba ya Grayson iliyovunjwa na imezungushiwa ukuta na geti kupigwa kufuli.
Hata hivyo, Uwazi lilifika katika Ofisi za Serikali ya Mtaa wa Bunju ‘B’ na kuonana na mtendaji Abdallah Mkeyenge ambaye alikiri kuwepo kwa mvutano baina ya watu hao.“Hii barua ya makubaliano ya kuuziwa Grayson kiwanja inaonekana imetoka ofisini hapa lakini mimi kipindi hicho nilikuwa sijahamia ofisi hii.
Jumba la kifahari la Mch. Getrude Rwakatare.
“Ninachokumbuka kuna kipindi Mchungaji Rwakatare alikuja na milioni tano kuwapa Grayson na mtu mwingine yaani kuwapoza lakini walikataa kuzichukua,” alisema mtendaji huyo.
Mchungaji Rwakatare alipopigiwa simu kuhusiana na madai hayo alisema yupo bungeni hivyo alimwagiza msaidizi wake, Jerad Abeid kuzungumzia sakata hilo ambapo alisema eneo hilo mchungaji analimiliki  tangu mwaka 2005 na hati ziko ardhi Wilaya ya Kinondoni. Alibomoa nyumba ya Grayson akijua ni eneo lake la siku nyingi.
“Unajua katika maeneo hayo kuna watu walikuwa wakishirikiana na ofisi za mtaa kuuza kiwanja cha mchungaji kwa siri na tayari watu wanne walishauziwa lakini walikuwa hawajajenga,  mchungaji aliamua kuwapoza kiubinadamu na wameshaondoka bado watu wawili akiwemo huyo Grayson,” alisema Jerad.

0 comments:

Post a Comment

Pages