Albino Wawaliza Maaskofu 10 na Mashehe 10 Katika Hospitali ya Bugando
Viongozi wa madhehebu ya dini jijini Mwanza, wakiwamo Maaskofu na Mashehe jana walijikuta wakibubujikwa na machozi baada ya kumtembelea Ester John, ambaye amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Ester
amelazwa baada ya kujeruhiwa vibaya na watu wasiofahamika, ambao
walimteka mwanawe mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Yohana Bahati na
kutokomea naye kusikojulikana.
Viongozi
hao wakiwemo maaskofu 10 na mashehe 10 walimtembelea Ester hospitalini
hapo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kongamano kubwa la amani
linalotarajiwa kufanyika Februari 28 mwaka huu kuiombea nchi amani na
kulaani mauaji ya albino.
Mashehe
na maaskofu hao walimuombea dua na sala Ester aweze kupona haraka na
walilaani kitendo cha kinyama, alichofanyiwa na wauaji hao.
Waliiomba Serikali ichukue hatua za haraka kukomesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini.
Akizungumza
hospitalini hapo huku akitokwa na machozi katika Wadi Namba 9
alikolazwa Ester, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa ya
Viongozi wa Dini, Shehe Hassan Kabeke alisema wanaungana kwa pamoja
kulaani matukio mawili ya kinyama ya kuuawa kwa mtoto Yohana na
kujeruhiwa vibaya mama yake mzazi.
“Maneno
ya kusema yananiishia baada ya kumuona Ester, mimi nadhani hakuna
sababu ya kuremba maneno dhidi ya ukatili huu wa kinyama, nasikia
maumivu makali sana ndani ya moyo wangu kama kiongozi wa kiroho,
tunaitaka serikali katika hili isiondoe adhafu ya kifo kwa kisingizio
cha haki za binadamu”, alisema.
Aliongeza “Tunapozungumzia
haki za binadamu, maana yake ni usawa, ukweli na haki kwa watu wote
nchini, haiwezekani watu wengine waue watu halafu tunasingizia haki za
binadamu, na wao wahukumiwe adhabu ya kifo, katika hili msimamo wetu
kama viongozi wa dini tunaomba adhabu ya kifo isiondolewe”.
Pia,
aliwataka majaji wanaosikiliza kesi za watu wenye ulemavu wa ngozi,
kuzisikiliza kwa wakati ili kuondoa ucheleweshaji wa kesi hizo ili
hukumu zitolewe kwa wakati.
“Nichukue
fursa hii kwa niaba ya wenzangu kuwaomba waheshimiwa majaji waharakishe
kusikiliza mashauri yaliyoko mahakamani yanayohusisha mauaji ya watu
wenye ulemavu wa ngozi (albino)”, alisema.
Kwa
upande wake, Katibu Mwenza wa Kamati hiyo ya Amani, Askofu Zenobius
Isaya alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu
kulichukulia suala la mauaji ya albino kwa uzito wa kipekee kwa vile
linagharimu maisha ya watu wasio na hatia katika jamii.
“Tunamuomba
IGP Mangu alichukulie suala hili kwa uzito mkubwa, afanye uchunguzi wa
kina ili aweze kukomesha mauaji haya ambayo yameipaka matope nchi yetu
mbele ya Jumuiya ya Kimataifa”, alisema.
Akitoa
salaam kwa Ester ambaye aliweza kukaa kitandani kwa muda, Isaya alisema
shida iliyomkuta ni shida ya Watanzania wote wenye kupenda amani na
kuchukia maovu.
“Shida
iliyokukuta na taabu yako ni taabu yetu sisi sote wapenda amani ; na
sisi wapenda amani kwa wingi wetu, kama unavyotuona, tunalaani tukio
hili la kinyama, jambo hili ni la kinyama lakini tunakutia moyo uweze
kupona haraka na Mungu akupe moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki
kigumu,” alisema.
Aliushukuru
uongozi wa Hospitali ya Bugando kwa kufanya kazi kwa uvumilivu na
kutanguliza upendo katika kumhudumia Ester tangu alipolazwa hospitalini
hapo Februari 17 mwaka huu.
“Nichukue
fursa hii kuwashukuru sana madaktari na wauguzi wetu kwa kuwa bega kwa
bega na Ester kwa kumhudumia bila ya kuchoka, hii inaonyesha kuwa na
mshikamano na Mungu awabariki”, alisema.
Awali,
akiupokea ujumbe huo, Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa Hospitali ya
Bugando, Leah Kagina aliwashukuru viongozi hao wa dini kwa kuamua
kutenga sehemu ya muda wao kwa kwenda kumjulia hali.
Alisema hiyo ni mara ya kwanza kwa hospitali hiyo kupokea ujumbe huo mkubwa kwenda kumjulia hali Ester.
“
Tunawashukuru sana kwa ujio wenu, ni kwa mara ya kwanza kwa hospitali
kupokea ujumbe huu mzito wa viongozi wa kiroho kwa ajili ya kuja
kumjulia hali Ester, hii inadhihirisha ni jinsi gani mlivyo na upendo
kwa watu wote, rai yangu kwenu niwaombe mtumie ibada zenu katika kutoa
elimu kwa jamii dhidi ya mauaji haya”, alisema.
Alisema
kuwa viongozi wana nafasi kubwa katika kuelimisha jamii juu ya imani
potofu, ambazo zimekuwa zikienezwa dhidi ya mauaji hayo na kuitaka
serikali kuwachukulia hatua stahiki wauaji wa watu wenye ulemavu wa
ngozi.
Akizungumzia
hali ya mgonjwa, Muuguzi wa Zamu katika wadi Namba 9, alikolazwa Esta,
Adolphina Kishumba alisema hali ya Ester kwa sasa inaendelea vizuri na
anajitahidi kula chakula.
“Kwa
hivi sasa hali ya Ester inaendelea vizuri, ni tofauti na alivyokuwa
mwanzo na sasa hivi anakula na anaanza kutembea kwenda chooni”, alisema.
Mama
mzazi wa Ester ambaye anamuuguza hospitalini hapo, Tabu Mang’enyi
aliwashukuru Watanzania kwa misaada yao ya hali na mali wakati wote,
ambao amekuwa na mwanawe hospitalini hapo.
“Nawashukuru
Watanzania wote kwa kumuombea mwanangu na kuendelea kumjulia hali.
Kutokana na maombi yenu hali ya mwanangu inaendelea vizuri”, alisema.
0 comments:
Post a Comment