Chenge, Tibaijuka Kikaangoni Baraza la Maadili Wiki hii
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge Jumatano atasimama mbele ya Baraza la Maadili kujibu tuhuma za kukiuka maadili ya uongozi na kujipatia Sh bilioni 1.6 ambazo aligawiwa kutoka katika fedha za akaunti ya Tegeta Escrow.
Profesa
Anna Tibaijuka ambaye alitimuliwa Uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi
kutokana na kujipatia Sh bilioni 1.6 kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya
VIP Engineering, James Rugemalira atajibu tuhuma hizo Alhamisi.
Ratiba
iliyotolewa na Baraza la Maadili, jijini Dar es Salaam inaonesha kuwa
aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, William
Ngeleja ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema, atasimama mbele ya Baraza
hilo Jumatatu ijayo.
Wengine
watakaopanda kizimbani ni Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma atakayehojiwa
Jumatatu ijayo.
Wengine
ni Mnikulu Shaban Gurumo atakayehojiwa Machi 4, akifuatiwa na
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Ufilisi na Udhamini (RITA), Philip
Saliboko na Machi 6 atahojiwa Naibu Kamishna Upelelezi na Kodi Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), Loicy Appollo.
Ratiba
hiyo inaonesha kuwa Machi 9 atahojiwa Mkurugenzi Mdhibiti Uchumi
Mamlaka ya Usafiri wa Anga, Dk Benedict Diu akifuatiwa na Meya wa
Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Gulam Remtullah.
Akizungumza
Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji mstaafu Hamis Msumi
alisema ratiba ya kuwahoji viongozi, ilitakiwa kuanza jana ikianza na
aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo. Hata hivyo, Gambo
aliwasilisha barua kwamba anaumwa na atashindwa kuhudhuria.
Vievile,
Gambo aliwasilisha cheti cha daktari akitakiwa kupumzika kwa wiki
mbili, jambo lililosababisha Baraza hilo kuahirisha kusikiliza shauri
lake hadi hapo litakapopanga kikao kingine.
Kutokana
na kuanza kuwapandisha kizimbani watuhumiwa wa sakata la Escrow,
Baraza litatoa uamuzi wa ama wahusika hao wafikishwe mahakamani, au la,
kulingana na hatia watakazokutwa nazo.
Kashfa
ya Escrow iliyonguruma mwaka jana bungeni, imesababisha baadhi ya
watuhumiwa kujiuzulu nyadhifa zao na wengine kuvuliwa madaraka, akiwamo
Profesa Tibaijuka aliyewekwa pembeni na Rais Jakaya Kikwete Desemba
mwaka jana.
Chenge
alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na aliachia wadhifa huo
hivi karibuni. Ngeleja aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Katiba, Sheria na Utawala na Mbunge wa Lupa na Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Nishati na Madini , Victor Mwambalaswa, nao walijiuzulu hivi
karibuni.
Chenge
na Profesa Tibaijuka kila mmoja alipata mgawo wa Sh bilioni 1.6 huku
Ngeleja akipata Sh milioni 40.4 kutoka kwa James Rugemalira wa VIP
Engineering and Marketing Limited, zikiwani mgawo wa Tegeta Escrow.
Akaunti
ya Tegeta Escrow ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mwaka 2006
kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya uwekezaji (capacity
charges), zilizokuwa zinalipwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO)
kabla hazijakabidhiwa kwa anayelipwa, ambaye ni Kampuni binafsi ya kufua
umeme ya IPTL.
0 comments:
Post a Comment