Namna ya kuifanya simu yako idumu na chaji muda mrefu
Simu hizi ni sawa na kuwa na kompyuta ya kawaida iliyounganishwa na mtandao wa intaneti.
Kwa mfano, simu hizi zinakupa nafasi kubwa ya
mawasiliano kupitia mitandao ya kijamii ya WhatsApp, Facebook, Skype,
Viber, Kik Messenger, Twetter, WeChat, LinkedIn, Badoo, Instagram na
Twoo.
Pia simu za kisasa zina huduma mbalimbali zikiwamo
za kujua jiografia ya maeneo, vipimo vya joto, mapigo ya moyo, upigaji
wa picha na huduma nyinginezo.
Kwa kutumia mitandao ya kijamii watu sasa hawana
sababu ya kujisika wapweke, kwani hata ukiwa chumbani peke yako unaweza
kuungana na watu duniani kwa kujadili na kupokea taarifa mbalimbali.
Hivyo simu hizi zimeweza kuwakusanya watu waliotawanyika sehemu mbalimbali na kujadili mambo kama vile wamekusanyika eneo moja.
Mbali na hilo, simu nyingi zina uwezo mkubwa wa
kasi ya mawasiliano ya intaneti, hivyo kuwa rahisi kutuma na kupokea
barua pepe na kupata taarifa kutoka tovuti mbalimbali duniani.
Ni kutokana na mambo hayo, simu hizi zimeonekana ndizo za kisasa na watu wengi wameamua hata kujinyima ili kuzinunua.
Kasoro ya simu hizi
Pamoja na watu wengi kuzipenda, simu hizi zimekuwa
ni kero kutokana na uwezo mdogo wa betri zake kudumu na chaji au nguvu
za kuziendesha. Awali watu wengi walipenda simu zinazodumu na chaji muda
mrefu.
Simu za kisasa zina udhaifu wa kushindwa kudumu na
chaji. Nyingi zinatumika kwa saa sita hadi 12. Kwa sababu hii watumiaji
wengi wameamua kununua vifaa vya kuhifadhia umeme kwa ajili ya
kuzichaji. Vifaa hivi vinajulikana kwa jina la’ power banking’
Kinachokuonyesha kuwa uwezo unapungua ni pale
unapojikuta siku za mwanzo unachaji kwa siku moja baadae mara mbili kwa
siku, mara tatu na hatimaye unajikuta unachaji mara kwa mara.
Kwanini simu hizi hazidumu na chaji kwa muda mrefu kama zilivyo
simu nyingine? Nini kifanyike ili kutatua tatizo hili? Wataalamu wana
majibu.
Sababu za kuisha chaji mapema
Mmoja wa waanzilishi wa Kampuni ya Farbe Tecnik
inayojihusisha na utengenezaji wa vifaa vya kuchaji simu, Shane Broesky
anasema kupungua kwa uwezo wa kuhifadhi chaji kwa simu hizi ni uzembe wa
watumiaji.
Anasema watu wengi hudhani kuziacha simu zao
zikiwa zinachajiwa usiku mzima au kwa muda mrefu ni kupunguza uwezo wa
betri kuhifadhi umeme.
Broesky, katika maelezo yake aliyoyatoa kupitia
mtandao wa Digital Trends, anawatoa hofu wamiliki wa simu kuwa kuziacha
kwenye chaji kwa muda mrefu hakuharibu simu zao.
Anafafanua kuwa hii ni kwa sababu simu hizo zina
mfumo mzuri wa kuzuia umeme usiendelee kuichaji betri baada ya kufikia
kiwango cha juu cha asilimia 100.
Broesky anasema hii inasaidia kuepusha betri
kuchajiwa kupita kiasi. Lakini akasema kitendo cha kuicha kwenye mfumo
wa kuchaji, kinasababisha kila betri ikipungua kidogo kutoka kiwango cha
juu, ianze kuchajiwa tena.
Kitendo hicho kinapojirudiarudia, anasema ndiko
kunakoua uwezo wa betri hasa zile za aina ya ‘Lithium-ion’ katika
kuhifadhi umeme.
Anasema betri hizi zinapokuwa na kiwango cha juu cha umeme, ikichajiwa joto lake linapanda.
“Kitendo cha betri kuwa kwenye hali ya joto kwa
muda, ndiko kunakoharibu uwezo wake wa kudumu na umeme kwa muda mrefu,’’
anasema.
Namna ya kuwezesha chaji kudumu
Ili betri ya simu yako iendelee kuwa na uwezo,
Broesky anasema unapaswa uichaji kwa kiwango cha kati ya asilimia 50 na
80. Ukitumia mfumo huo, utaifanya betri ya simu yako iendelee kuwa na
uwezo wa juu wa kudumu na umeme kwa muda mrefu.
Jambo lingine la kuifanya betri yako idumu na umeme ni kuepuka betri yako kupungua umeme hadi simu kuzima.
Kampuni ya Simu ya Tecno nayo ilitoa taarifa
kwenye mtandao wake kuwa mtumiaji wa simu za kisasa anapaswa kuepuka
simu yake kupata moto wakati wa matumizi.
Taarifa ya kampuni hiyo ambayo simu zake
zinaonekana kutamba katika soko hapa nchini, inaelezea kuwa iwapo
unatumia intaneti katika mazingira ya mawasiliano hafifu, simu hupata
moto.
Inawashauri watumiaji wa simu hizo pia wasiziache
zikiwa zimefunguliwa ukurasa wa mawasiliano ya intaneti kwa sababu
wakati mawasiliano yanakuwa madogo, hupata moto.
0 comments:
Post a Comment